Saturday, November 8, 2008

Watuhumiwa zaidi wapelekwa mahakamani

Na Pauline Richard na Ramadhan Semtawa -Kutoka Mwanachi


MTEGO wa ufisadi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), umeendelea kunasa watuhumiwa, na safari hii umewazoa wafanyakazi wanne wa benki hiyo ambao wamefikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kujibu tuhuma hizo.
Kwa idadai hiyo sasa watuhumiwa wa ufisadi huo waliokamatwa na kupandishwa kizimbani wanafikia 17.
Watuhumiwa waliofikishwa mahakamani jana walitakiwa kujibu madai ya kuisababishia BoT hasara ya zaidi Sh2.2 bilioni za EPA.
Mwendesha Mashtaka wa serikali, Wakili wa Boniface Makulilo aliwataja watuhumiwa waliofikishwa mahakamani hapo kuwa ni Esther Leon ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Madai ya Biashara, Iman Mwakosya na Sophia Joseph ambao ni Wakuu wa Idara ya Madeni ya Biashara katika Benki hiyo.
Watuhumiwa hao wameunganishwa na mtuhumiwa Rajabu Malanda ambaye juzi alisomewa shtaka lake mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Anyimilile Mwaseba na jana alipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Warialwande Lema wa mahakama hiyo kwa kesi hiyo.
Katika kesi hiyo, Malanda alisomewa mashtaka sita na wafanyakazi wa BoT walisomewa shtaka moja la kuwa wazembe wakiwa kazini na kusababisha hasara ya kiasi hicho cha fedha.
Malanda alidaiwa kughushi hati bandia ya usajili iliyokuwa inaonyesha imetolewa na usajili wa Kampuni ya Manner Planner Consultant na kujipatia zaidi ya Sh2.2 bilioni.
Ilielezwa mahakamani hapo kuwa Novemba 29, 2005 Malanda aliwasilisha hati ya uongo katika Benki ya Biashara (Commercial Bank of Africa) iliyokuwa inaonyesha kuwa wao ni wamiliki wa Kampuni ya Manner Planner .
Mtuhumiwa baada ya kuwasilisha hati hiyo inadaiwa alihamishia deni hilo katika Kamapuni ya B Grancers Company Limited ya Ujerumani na Kampuni ya Monner Planner ya Tanzania, baada ya kuonyesha hati hiyo, iliyokuwa imesainiwa na Jonas Banji na Fundi Kitunda kwa madai kuwa wao ni wakurugenzi wa kampuni hizo.
Katika shtaka jingine inadaiwa Novemba2, 2005 mshtakiwa Malanda na Farijala Husein waliwasilisha hati ya uongo ya Kampuni ya BG Monner ambayo ilikuwa inaonyesha kuwa imesainiwa na Mkurugenzi wa Makampuni na kuiwasilisha BoT.
Baada ya kuwasilisha hati hiyo BoT, watuhumiwa hao walijipatia zaidi ya Sh2.2 bilioni mali ya BoT.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Desemba 7 mwaka 2005 watumishi hao wanadaiwa kufanya uzembe na kusababisha hasara kwa mamlaka maalumu ya Benki hiyo wakiwa kama wakurugenzi wa idara ya madai wa BoT.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa wote walikana kuhusika na tuhuma hizo na mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 13 mwaka huu watakaposomewa maelezo ya awali, baada ya upande wa mashtaka kueleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Watuhumiwa wote wamerudishwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Watumishi hao wa BoT wametakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini dhamana ya Sh450 milioni na kwamba hawatatakiwa kusafiri nje ya Dar es Salaam pamoja kuwasilisha pasipoti zao za kusafiria mahakamani hapo.
Wakati moto huo ukiwawakia watuhumiwa hao huku wakidaiwa kutoroka, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba, amesema watuhumiwa watafikishwa mahakamani mmoja baada ya mwingine.
Kauli ya DCI ambaye kurugenzi yake ndiyo yenye mamlaka ya kukamata wahalifu baada ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kutoa kibali, imetolewa wakati Watanzania wakitaka kuona watuhumiwa wote wa fedha za EPA zaidi ya Sh 133 bilioni wanakamatwa.
Hadi jana mchana, mmoja wa watuhumiwa ambaye amesomewa mashtaka bila kuwepo mahakamani kwa madai yuko nje ya nchi, Mwesiga Lukaza alikuwa bado hajakamatwa.
Akizungumzia mtuhumiwa huyo na mchakato wa kuwakamata wahusika, Manumba, alisema ni suala la wakati tu kwani hakuna mtu atakayepona.
Mwesiga na ndugu yake Johnson Lukaza, wote wanakabiliwa na makosa sita, ambayo ni pamoja na kughushi nyaraka kwa kutumia Kampuni ya Kernel Limited of Tanzania na Marubeni Corporation ya Japan na kujipatia mabilioni ya fedha.
Hata hivyo, ni Jonhson ndiye aliyefikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka hayo huku Mwesiga akiwa bado kupatikana akidaiwa kwamba yuko nje ya nchi.
Akizungumzia zaidi hilo, Kamishna Manumba alisema; "Sipendi kusema sana kwani yupo kiongozi wetu ambaye ni DPP (Eliazer Feleshi), lakini ninachoweza kusema ni kwamba, ni suala la wakati tu, hakuna mtu atapona," alionya Kamishna Manumba na kuongeza:
"Kama mnavyoona tunawapeleka watu kwa ‘phase’ (awamu), lakini DPP ndiye anayefahamu zaidi nani atapaswa kwenda lini, sisi kazi yetu ni kuwakamata tu."
DPP Feleshi alipoulizwa kuhusu mchakato wa kuwafikisha mahakamani, alisema kinachofanywa na ofisi yake sasa kinaonekana mahakamani kila siku na huko ndiko utakaojulikana ukweli.
DPP Feleshi kama alivyo Kamishna Manumba, ambao wote huwa na ushirikiano mzuri na vyombo vya habari, alisema ameona sasa azungumze kwa vitendo si maneno.
"Sasa hivi kila kitu kinafahamika mahakamani, maana sipendi kuzungumza maneno mengi zaidi ya yale yanayojiri mahakamani kila siku, ni vitendo tu si maneno," alifafanua DPP Feleshi.
Alisema, huu si wakati wa kutoa maneno mengi nje ya mahakama, kwa sababu mchakato huo sasa unafanyika kortini, ambako mambo yote hujibainisha.
Kauli za vigogo hao wa wawili kutoka upande wa mashtaka na polisi, zimetolewa wakati kila siku kuna watu wapya wanakamatwa kwa tuhuma za ufisadi wa EPA na kupelekwa mahakamani.
Maelezo hayo ya DCI na DPP yanazidi kuwaweka watuhumiwa wa EPA katika wakati mgumu, wakiwemo wale waliorejesha zaidi ya Sh69 bilioni ambao wanadhani wamesamehewa.
Kauli hizo pia zinazidi kuwaweka mafisadi wa EPA katika hali tete, kutokana na duru za kiserikali kuonyesha kwamba fedha zilizorejeshwa huenda zikawa kidhibiti cha kukamata watu hao kwa urahisi kwamba walihusika na ufisadi.
"Si kwamba wamekwisha, bado mzee, mambo taratibu, mchakato unaendelea na wananchi wataona, serikali imejipanga vizuri katika hili," kilisema chanzo hicho.
Ufisadi ambao umebainika katika hesabu za BoT za mwaka 2005/06, unahusu Sh90.3 bilioni ambazo ziliibwa na makampuni 13 kwa kutumia nyaraka za kughushi.
Pia unahusu Sh42.6 bilioni zilizolipwa kwa makampuni tisa, katika mazingira yenye utata huku taarifa nyingine za wizi huo zikiwa nje ya nchi, hali iliyomfanya Rais kuongeza muda wa uchunguzi kutoka Agosti hadi Oktoba 31.